Jinsi ya kuingia kwenye uandishi wa vitabu


Jinsi ya kuingia kwenye uandishi wa vitabu

Kwa mfano, mwalimu anayefundisha shuleni au chuoni atakuwa na hamu ya kuandika kitabu lakini atajiuliza, “naanzaje?”, mtangazaji wa redio au runinga naye atajiuliza swali hilo hilo, “naanzaje?”. Kujiuliza swali hili haimaanishi mtu hawezi kuandika kitabu ila kwa kutumia mazingira aliyopo, anaanzaje kuandika kitabu?.

Kama wewe ni mtu ambaye umekuwa ukitamani kuandika kitabu, pengine una wafuasi wengi mtandaoni na wanataka kitabu chako, au mtangazaji redioni na watu wanauliza kitabu chako, au unapenda kuandika kuandika lakini hujaweza kuandika kitabu na kuwafanya wafuatiliaji wa machapisho yako kufurahi, basi kwa kusoma andiko hili mpaka mwisho utafahamu namna ya kuanza kutokea hapo ulipo na hatimaye ukawa na kitabu chako. Nimegawanya watu wanaotaka kuandika kitabu katika makundi matano ili kukusaidia ujijue upo ndani gani na utumie njia ya kukufaa katika kundi lako. Makundi haya ni kama ifuatavyo;

1. Watu wanaopenda kuandika kuandika

Kuna watu wanapenda kuandika andika sana ila wameshindwa kuendelea mbele na kutoa vitabu vyao. Watu walio katika kundi hili wanahitaji kusukumwa kidogo tu kwa sababu tayari wana contents, kilichobakia ni kumalizia hatua moja ndogo tu ya mwisho. Kama wewe upo hapa, unamaliziaje sasa?.

Si unaandika machapisho mazuri mtandaoni (Facebook, WhatsAPP, Instagram na n.k)?, Kama si mtandaoni, si unaandika machapisho mazuri na kuyaweka kwenye blog yako? Pengine hata unawaandikia wengine vitabu vyao na kushiriki mashindano ya uandishi? Kama ndio, sasa fanya hivi; endelea kuandika na chagua eneo moja ambalo utaandika zaidi tena iwe lile unalolipenda zaidi, chomoa vipande vidogo vidogo na viposti mtandaoni au kwenye blog yako kama kawaida. Ukimaliza kukusanya, tayari una kitabu!.

2. Watu ambao ni waraghbishi na wajasiriamali

Kuna watu ambao tunawaita ni waraghbishi. Hawa ni watu wenye sauti kubwa mtandaoni kwa sababu ya ushawishi walionao kwa mashabiki wanaowafuatilia. Halafu kuna kundi lingine la watu ambao ni wajasiriamali. Sasa, hawa wote wanawezaje kuingia kwenye uandishi wa vitabu, pengine wewe upo kwenye kundi hili na umekuwa na hamu ya kuwa na kitabu.

Waraghbishi na wajasiriamali wengi hufanya podikasti, siyo? Wengine hualikwa kwenye semina na warsha kutoa speech na keynote, siyo?. Safari ya kuandika kitabu huanzia hapo!.

Tumia podikasti, speeches na keynotes unazotoa kuzibadilisha kuwa kitabu, hivi ndivyo utakavyoingia kwenye uandishi wa vitabu. Huhitaji kuzunguka sana na kujiuliza utafanyaje, anzia hapo kwenye podikasti zako, speeches zako au keynotes zako.

Unapoandaa kitu cha kuzungumza kwenye podikasti yako, unapoandaa keynote ya kuzungumza mahali ulipoalikwa, hayo ndiyo mazoezi yenyewe ya kuandika kitabu. Ukifanya podikasti huwezi shindwa kuandika kitabu.

Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba, kwa waraghbishi na wajariamali, staili yao ya kuingia kwenye uandishi wa vitabu ni kupitia kile wanachofanya tayari, yaani podikasti zao, speeches zao au keynotes zao

3. Walimu wote kwa ujumla wao

Kutaja kwa uchache hapa, inagusa walimu wa chuo, shule, wale wanaofundisha kanisani, msikitini na kadhalika. Hawa tayari wanaandika na kama upo kwenye kundi utakubaliana na mimi. Kuna mwalimu asiyeandaa vitini? Kuna ambaye haandai makala na mawasilisho mbalimbali? Tena wakati mwingine huombwa kuandika dibaji za vitabu vya watu wengine lakini wao wanabaki kujiuliza “nitaandikaje kitabu changu?”.

Sasa iko hivi, mwalimu yeyote anaingia kwenye uandishi kupitia vitini, makala na mawasilisho anayoandika!. Kama wewe upo kwenye kundi hili, ni wakati sasa uanze kubadilisha hivyo vitini kuwa kitabu, hizo makala kuwa vitabu, ni rahisi tu!

Staili yako ya kuingia kwenye uandishi ndiyo hiyo. Tayari una mazoezi ya kutosha ya kuandika, si kila siku unaandika?.

4. Wabobezi na watu maarufu

Walio kwenye kundi hili wanaingiaje kwenye uandishi wa vitabu? Au kwa lugha rahisi niseme hivi, “wataandikaje vitabu vyao”?. Kama wewe upo kwenye kundi hili, staili yako ya kuingia kwenye uandishi wa vitabu ni hii hapa; kwa wale wabobezi, watu ambao ni mabingwa kwenye eneo fulani, kupitia makala na machapisho ambayo wataandika kueleza ujuzi wao, wanaweza kugeuza hizo makala kuwa vitabu pia.

Kuna watu maarufu kama vile watangazaji wa runinga na redio, hawa huandaa vipindi mbalimbali. Zile contents za kwenye kipindi ndiyo kitabu chenyewe.

5. Wenye ndoto tu peke yake

Kuna watu wana ndoto za kuwa na vitabu vyao lakini hawawezi kuandika kabisa. Kama upo kwenye kundi hili, dalili ya kwanza ni kwamba hupendi kuandika kuandika lakini una ndoto kubwa ya kuwa na kitabu. Sasa, unaingiaje kwenye uandishi wa vitabu?

Kama upo kundi hili, wewe utaingia kwenye uandishi wa vitabu kwa kutumia njia ya kuandikiwa na mtu mwingine. Watu wanaoandikia wengine vitabu huitwa mwandishi fichwa (ghostwriter). Kaa na ghostwriter na mweleze kitabu unachotaka kuandika ila huwezi kuandika kisha yeye sasa akiandike. Kwa staili hii utakuwa umeingia kwenye uandishi wa vitabu.

Hitimisho

Kuingia kwenye uandishi wa vitabu sio kazi kubwa kama utaanzia kwenye kile unachokifanya. Ninaposema “kuingia kwenye uandishi wa vitabu” namaanisha uwe na kitabu chako ambacho mwandishi ni wewe!. Kwa hiyo basi, huhitaji kusema “sasa ngoja nikae nitenge muda niandike kitabu”, wewe tumia yale ambayo umekuwa ukiandika na kugeuza kuwa kitabu, iwe ni makala, mawasilisho, keynotes, podikasti na kadhalika.

Ukishamaliza hatua hii endelea na hatua inayofuata, unaifahamu? Kama siyo, wasiliana nasi upate usaidizi zaidi.

Credits: DL Bookstore

.